Thursday, 22 March 2018

W WAPO Social Media

APANDACHO MTU NDICHO AVUNACHO

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

“Msidanyanyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” (Galt.6:7)

Andiko la mada ya leo linatutahadharisha moja kwa moja bila kumung’unya maneno. Linaanza na “msidanganyike…” Muktadha wa usemi huu ni sawa na kusema, “msikubali kudanganyika, au kuhadaika, au kushawishika kwa uongo mkaugeuza kama ndio ukweli.”

Onyo hili linalenga kuhusu mambo ambayo kwa asili sivyo yalivyo ila yamenakshiwa kwa juu juu sura tofauti na uhalisia wake, kiasi cha kumfanya mtu asiyejali uhalisia wa kitu anaamua kuyaachilia mambo yaendelee kuwa ndivyo sivyo. Kwa hiyo, onyo la “msidanganyike” linatuepusha kuruhusu hali ya udanganyifu kushika hatamu nafsi mwetu kwa niaba ya ukweli katika mambo ya Mungu.

Onyo la pili tunalokutana nalo katika andiko la mada yetu ni: “Mungu hadhihakiwi”!!! Maana yake ni kusema kwamba: “Kamwe Mungu hataruhusu hali ya kudharauliwa, au kufanyiwa kejeli kwa sababu za chuki binafsi dhidi yake; na pia Mungu hataruhusu sheria na kanuni zake alizoziweka zipuuzwe na kufanyiwa utani wala mzaha na kuzikanyaga hovyo kama vile hakuna madhara yoyote.”

Katika uchambuzi nilioufanya kuhusu maonyo mawili yaliyotangulia katika andiko la mada yetu ya: “msidanganyike, Mungu hadhihakiwi…” kama ukiamua kutumia akili za kibinadamu unaweza kuona kweli ni maneno mazito na makali kwa tafsiri yake; lakini huuoni moja kwa umoja ukali wa Mungu katika uhalisia wake!

Maana sote tu mashahidi tukiona jamii ya walimwengu jinsi wasivyokuwa na hofu, heshima na adabu ambayo Mungu alistahili kupewa. Isitoshe ndio kwanza maelfu ya wengi hata wajitao waamini Mungu wanapoteza umakini katika mambo ya Mungu na wanaendelea kumdhihaki, kumtukana, kumdharau na kumkejeli Mungu kana kwamba hayupo kabisa!

Je! Mungu ni mwongo? Au hayupo kama “Wapumbavu” wengine wanavyojidanganya na kudanganyana? Kuna ushahidi gani unaoonyesha kweli Neno la Mungu ni kweli na linamaanisha kile lisemacho?

KIGEZO CHA KUPIMA KAMA MUNGU HADHIHAKIWI

Majibu ya maswali tata tunayapata kutoka kwenye tafsiri ya maneno yaliyosalia kwenye andiko la mada yetu ambayo ni: “….cho chote apandacho mtu ndicho atakachovuna..”! Mungu kwa hekima zake za Uungu, amejiwekea mfumo wa udhibiti wa kulinda heshima yake na maneno yake pasipo yeye Mwenyewe kujitokeza waziwazi kujitetea.

Mfumo wa udhibiti umewekwa kwenye kanuni za asili na kanuni za kimaumbile. Mathalan, kanuni ya uzalishaji wa mimea, Mungu ameweka mfumo wa udhibiti wa uumbaji wake kwenye mbegu. Kila mbegu inayopandwa ardhini itaotesha mmea wa mbegu husika, na kutoa mazao ya mbegu husika. Huwezi kupanda matikiti maji utarajie kuvuna nyanya! Huwezi kupanda ngano utarajie kuvuna mpunga hata kama vinafanana-fanana. Kwanini? Kwa sababu uumbaji asilia wa Mungu umedhibitiwa na Mungu mwenyewe kupitia mfumo wa kila mbegu aliyoiumba itoe mazao ya mbegu husika.

Japokuwa siku hizi kuna teknolojia za ujanja wa kujaribu kuigiza na kukosoa kazi ya uumbaji wa Mungu kwa kujaribu kutengeneza vitu mbadala vyenye kufanana na vitu asilia; ukweli unabaki pale pale bado ulaghai nao unaheshimu kanuni zile zile, yaani ukitumia ulaghai atavuna ulaghai vile vile! Kitu bandia au feki hakiwezi kuzalisha kitu halisi na asilia! Haiwezekani. Kwanini? Kwa kuwa Mungu hadhihakiwi katika mambo ambayo yamo katika udhibiti wake!

TUNAPANDA MBEGU KILA SIKU NA TUNAVUNA TULICHOPANDA

Mungu ni mtakatifu sana, mwenyehaki na mtendahaki asiye na upendeleo wala ubaguzi dhidi ya mtu yeyote. Mungu hawezi kwenda kinyume na kanuni alizoziweka ndani ya Neno lake. Kiroho na kibiblia maneno ya vinywa vyetu ni mbegu zinazotumika kuzalisha matunda yatokanayo na maneno yetu. Kila uchaguzi tunaoufanya katika jambo lolote nao pia ni mbegu ambayo tunapokea matunda ya aina ya mbegu tuliyopanda kwa maana ya kupata matokeo ya uchaguzi tulioufanya wenyewe!

Kwa hiyo, Mungu anaposema “cho chote apandacho mtu ndicho atakachovuna..” ina maana ya “maneno yetu”, na “uchaguzi wetu” vinageuka kuwa mbegu tuzipandazo katika maisha yetu ya kila siku., na hivyo lazima tutarajie kupata matokeo ya maneno na maamuzi yetu. Matokeo ya mambo tunayokutana nayo, au yanayotupata, yawe mema au mabaya, vyote ni mazao ya mbegu za maneno na uchaguzi tuliofanya wakati uliopita. Tunapanda mbegu kila siku na tunavuna tulichopanda wakati uliopita.

Kwa mantiki hii, “uamuzi” ni mbegu! maneno ya vinywa vyetu ni mbegu! Kama uamuzi uliofanyika ni mbaya hata pasipo kujua, kanuni ya asili inazingatiwa na kuhakikisha mhusika anavuna matokeo mabaya ya uamuzi wake wa awali.

Mathalan, Tunasoma kwamba “Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.... Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” (Yh.3:16,18)

Katika maandiko haya kuna kanuni isiyodhihakiwa. Uchaguzi wa kila mtu ndio unatoa mwelekeo wa hatma ya kila mmoja wetu. Kanuni inasema “kila mtu amwaminiye asipotee…bali awe na uzima wa milele…” Hakuna awezaye kubadilisha kanuni hii isifanye kazi kwa kila mtu anafanya uamuzi wa kumpokea Yesu awe mwokozi wake binafsi.

Wakati huo huo, kanuni ina upande wa pili kwa “kila mtu asiyeamini”! Tumesoma ya kwamba “amekwisha kuhukumiwa kwa kutokumchagua Yesu kuwa mwokozi wake”! Na kila mtu aliyeko chini ya hukumu Mungu hawezi kumtetea wala kumlinda na mabaya kwa sababu tayari kanuni ya hukumu inatenda kazi dhidi ya muhusika kwa hiari yake mwenyewe!

ITAENDELEA SEHEMU YA PILI

Kama umebarikiwa na ujumbe huu, nijulishe kwa ku-like na pia uwarushie marafiki zako pia. Ubarikiwe sana!

 

LATEST VIDEOS

Newsletter

Subscribe to Wapo Mission International weekly Newsletter.

Do you need JESUS as your personal savior?
If YES then Click HERE
Please rate our website

Need To Reach Us?

Email:

info@wapo.or.tz

Phone:

|+255 766 777 126 |
|+255 713 649 865 |
|+255 712 249 724 |
Do you need JESUS? Click here

Who's Online

We have 20 guests and no members online