Thursday, 22 March 2018

W WAPO Social Media

Roho Mtakatifu ni zaidi ya Wachawi na Waganga wa Tunguri

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Naomba kuwasilisha mada tata hii inayohusu mambo ya wachawi na ya waganga wa tunguri, kwa sababu, sio siri hivi sasa hata makanisani uchawi ni tishio kinyume kabisa na imani ya Ukristo. Mada hii sio kukuelimisha tu bali kukukaribisha pia kwenye kupata ufumbuzi wa tatizo lenyewe. Umefika wakati sasa turudi kwenye msingi ya imani ya kweli katika Kristo ambapo kuna matokeo halisi badala ya kubaki katika itikadi za kimadhehebu ambazo hazina tija kwa wafuasi wake.

Tafsiri ya Misamiati ya Uchawi


Katika jamii ya kitanzania kuna majina yaliyoshamiri katika mazungumuzo yanayotajwa kwa misamiati ya “uchawi”, “uuguzi”, “unajimu” na “ushirikina”. Kabla sijaanza kuyachambua nianze kwanza na tafsiri ya misamiati yenyewe kama ifuatavyo:
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili sanifu neno “uchawi” limetafsiriwa kuwa ni: (i) Ufundi wa kutumia dawa au vitabu maalum vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe; sihiri,juju; (ii)Vifaa vinavyotumika katika shughuli za kurogea. Aidha, tafsiri ya neno ‘mchawi’ maana yake ni mtu anayesadikiwa kuwa anaweza kuwadhuhuru watu kwa kuwaroga; mlozi, kahini. Kutokana na tafsiri za maneno haya mawili ya ‘mchawi’ na ‘uchawi’ tunapata picha kwamba utamaduni wa lugha ya kiswahili unatambua na kukubali kuwepo kwa hali, vitendo na imani za kichawi.


Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu neno ‘Mwaguzi’ limetafsiriwa kuwa ni ‘mtu anayemtibu mgonjwa na kumponya’; au ‘mtu mwenye ujuzi wa kufasiri ndoto au kubashiri mambo yatakayokuja’. Kisha tukichuguza neno ‘uaguzi’ tunakuta limetafsiriwa kuwa ni i) Namna ya kubashiri mambo yatakayokuja au kutafsiri ndoto au ishara ii) Namna ya utoaji huduma agh ya dawa iii) Namna ya kutegua au kugangua uchawi

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu neno ‘mnajimu’ limetafsiriwa kuwa ni i)Mtu mwenye elimu ya mienendo ya nyota; ii) Mtu mwenye elimu ya kutabiri utokeaji wa matukio kulingana na elimu ya nyota. Halafu neno ‘unajimu’ limetafsiriwa kuwa ni i) Elimu ya nyota au ii) Kazi ya najimu; falaki Neno la mwisho ni ‘mshirikina’ ambalo limetafsiriwa kuwa ni mtu mwenye kuamini na kupenda mambo ya uchawi na mazingaombwe; na neno ‘ushirikina’ limetafsiriwa kuwa ni ‘tabia ya kuamini mambo ya mambo ya uchawi, mizimu nk.

Sheria ya Uchawi


Tanzania inayo sheria maalum ya uchawi ambayo anatoa tafsiri ya viashiria vya mtu mchawi. Navyo vimetajwa ya kuwa mchawi ni: “Mtu yeyote mwenye- i) Kwa kauli zake au vitendo vyake vinamtambulisha kuwa ana nguvu za uchawi; ii) Kufanya, kutumia, au kumiliki, au kujitambulisha kuwa anamiliki vitu vyovyote vya uchawi; iii) Kugawa kusambaza kwa yeyote kitu cha kichawi; iv) Kutoa ushauri kwa mtu mwingine kuhusu matumizi ya uchawi, au kitu chochote cha uchawi; v) Kutishia kwa kutumia uchawi, au kwa kitu chochote cha uchawi dhidi ya mtu yeyote au mali ya mtu yeyote.
Kwa mujibu wa sheria ya uchawi kila mtu afanyaye mambo haya anatenda kosa la jinai. Na kwa mujibu wa sheria ya uchawi kila mtu yeyote afanyaye kitendo kinyume chini ya sheria hii chenye kukusudia kusababisha kifo, maradhi, majeraha, au balaa kwa jamii yeyote, au tabaka la watu, mtu, au mnyama, au kusababisha uharibifu kwa mali yeyote atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka 7.

Utafiti Kuhusu nafasi ya Tanzania katika Uchawi Kimataifa

Tafiti zilizofanywa miaka ya hivi karibuni na baadhi ya vyombo vya kimataifa vya habari na utafiti ziliipandisha daraja Tanzania na kushika nafasi ya kwanza kwa umahiri wa kuamini katika uchawi kimataifa. Mojawapo ya taasisi zilizoitangaza Tanzania kwamba imekithiri kwa mambo ya uchawi ni Pew Research lenye makao yake Washington DC nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa zake inasadikiwa kwamba miongoni mwa nchi 19 za Kusini mwa Jangwa Sahara ya Afrika zilizofanyiwa utafiti Tanzania imeongoza kwa kuwa na idadi ya watanzania 93% wanaoamini katika uchawi. Nchi ya pili inayoifuatia Tanzania ni Cameroon ambayo idadi ya washirikina wake ni 78%. Wakati huo huo nchi jirani ya ikiwemo Uganda yenyewe ina 29%, ikifuatiwa na Kenya yenye 27%
Vitendo vya uchawi vinavyoongoza kwenye uchawi ni pepo wachafu, juju, matamko ya laana za kichawi, na ufundi wa kutoa dawa za kinga dhidi ya kurogwa na kuthamini sana utoaji wa kafara kwa mizimu.

Chombo kingine ambacho kilifanya utafiti wake ni CNN kwa kufanya mahojiano mbali mbali na kutangaza kwamba, 60% ya watanzania waliohojiwa wanaamini katika utoaji wa kafara kwa mizimu au pepo wachafu kwa imani ya kujikinga na vitisho vya kulogwa, na ikaongeza kusema kwamba waumini wengi wa dini za Kikristo na Kiislamu, pamoja na kuhudhuria kwa wingi kwenye majengo ya ibada; bado wengi wao wameshikilia imani za kienyeji za kiafrika

Roho Mtakatifu ana nguvu za kudhibiti Uchawi na kukomesha Washirikina

Kimsingi wachawi na waganga wa tunguri pamoja na wasomaji nyota, wote wanatumiwa na nguvu za pepo wachafu. Ndiyo maana waganga wa tunguri hupandisha majini, au maruhani na mizimu ili kuwatabiria watu mambo yao na kuwafanyia mazingaombwe na viini macho.

Lakini tukirejea katika maandiko matakatifu ya historia ya kanisa la kwanza, tunashuhudia jinsi mitume wa Yesu na wakristo wa kwanza walivyopambana ana kwa ana na wachawi wa enzi hizo na kuzivunja kazi zao kwa mamlaka ya jina la Yesu:
“…..Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana….. (MDO 13:6-12)
Ni kutokana na uhalisia huu jumapili hii, pale BCIC Mbezi Beach, nitaongoza ibada maalum ya mafundisho na maombezi ya Ujazo wa Roho Mtakatifu yenye kuambatana na watu kufunguliwa katika vifungo vya nguvu za uchawi, uganga wa tunguri na mambo ya unajimu.

Kwa wakazi wa DSM, inawezekana wewe mwenyewe binafsi ni mwathirika wa imani za uchawi na ushirikina, umetembelea kwa waganga wa tunguri lakini bado unaishi katika vifungo na mateso ya kimapepo na mizimu ya ukoo. Au unaye rafiki, au jamaa ambaye ni mwathirika wa mambo haya. Unakaribishwa wewe pamoja naye, kuhudhuria ibada maalum ya mafundisho na maombezi pale BCIC Mbezi Beach kwa ajili ya kupokea nguvu za Roho Mtakatifu atakayekuponya na kukupa kinga ya kweli na ya kudumu pasipo malipo yoyote. Kwa walioko mbali basi nawataarifu ya kuwa ibada hii itarushwa moja kwa moja kupitia ukurasa huu, na kwenye Youtube na kwenye tovuti ya WAPO MISSION INTERNATIONAL. Karibuni sana na ubarikiwe.

 

LATEST VIDEOS

Newsletter

Subscribe to Wapo Mission International weekly Newsletter.

Do you need JESUS as your personal savior?
If YES then Click HERE
Please rate our website

Need To Reach Us?

Email:

info@wapo.or.tz

Phone:

|+255 766 777 126 |
|+255 713 649 865 |
|+255 712 249 724 |
Do you need JESUS? Click here

Who's Online

We have 25 guests and no members online